Jakaya-Kikwete1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhakikisha kuwa Balozi mbali mbali za Tanzania nje ya nchi zinakuwa na Waambata wa Elimu kwa nia ya kukabiliana na kutatua matatizo ya wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika nchi mbali mbali duniani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa mabalozi wanaoziwakilisha Tanzania nje ya nchi ni kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania walioko katika nchi hizo, bila kujadili kama Watanzania hao wamepelekwa nje na Serikali ama wamekwenda huko kwa njia nyingine.
Rais Kikwete amefanunua mambo hayo wakati alipozungumza na viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu katika Algeria, nchi ambayo Rais Kikwete anaitembelea rasmi kwa siku tatu kuanzia jana, Jumamosi, Mei 9, 2015. Tanzania ina kiasi cha wanafunzi 370 katika Algeria kwa sasa.
Rais Kikwete alizungumza na viongozi hao wanafunzi kwenye siku ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Algeria usiku wa jana, Jumamosi, Mei 9, 2015.
Akizungumza na viongozi hao wa wanafunzi, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina wanafunzi wengi katika nchi mbali mbali duniani, wanafunzi ambao wanahitaji huduma mbali mbali za kibalozi na hivyo ni lazima itafutwe namna ya kurejea katika utaratibu wetu wa zamani wa kuwa na Waambata wa Elimu katika balozi mbali mbali za Tanzania nchi za nje.
“Ni lazima tuwe na Waambata wa Elimu kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya vijana ….wanafunzi wetu nje ya nchi. Kila ninapokwenda nakabiliana na matatizo kama haya mnayoniuliza nyie na mengine mengi na ya aina mbali mbali ya wanafunzi,” Rais Kikwete amwaambia wanafunzi hao mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.
Kuhusu nafasi ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje, Rais Kikwete amesema kuwa ni shughuli muhimu ya kila balozi wa Tanzania katika nchi mbali mbali kushughulikia matatizo ya Watanzania.
“Mabalozi wetu kushughulikia matatizo ya Watanzania ni wajibu wao iwe ni wale Watanzania wanaopelekwa nje na Serikali ama wale ambao kwa njia moja ama nyingine wamejikuta nje ya nchi hata kama hawakupelekwa na Serikali. Huu ndio wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alianza ziara rasmi ya Kiserikali ya Algeria jana kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
10 Mei, 2015