Social Icons

Monday 13 April 2015

Serikali yaombwa ruzuku vyuo binafsi vya uuguzi, ukunga.


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
Serikali  imeshauriwa kutoa ruzuku kwa vyuo vya uuguzi na ukunga vinavyomilikiwa na watu binafsi, ili kuongeza idadi ya 
wataalamu wa kada hiyo kwa lengo la kupunguza ama kumaliza vifo vya mama na mtoto.
 
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Chuo cha Uuguzi na Ukunga Profesa Richard Lema, kwenye mahafali ya saba ya stashahada na ya pili ya cheti kwa wahitimu wa uuguzi na ukunga toka chuo cha Massana, jijini Dar es Salaam.
 
Profesa Lema alisema iwapo vyuo binafsi vitapatiwa ruzuku na serikali kama inavyofanyika kwa vyuo vyinavyomilikiwa na misheni, kada ya uuguzi na ukunga itapata watumishi wengi, hivyo kuisadia serikali katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto nchini.
 
“Ni dhahiri hatuwezi kupunguza vifo vya akina mama na watoto bila ya wakunga wa kutosha kwani hawa ndio wadau muhimu wa kupunguza vifo vya akina mama na vitoto vichanga, na muhimili wa kutekeleza malengo ya namba nne na tano ya Milenia,” alisema.
 
Alisema tatizo linalovikumba vyuo vya ukunga na uuguzi vya watu binafsi kama hicho cha Massana, ni lile la wanafunzi wa fani hiyo kushindwa kuendelea kutokana na tatizo la ada, pale wafadhili wao wanapojitoa kutokana na sababu mbalimbali.
 
Alisema tatizo hilo linaweza kutatuliwa na serikali kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na kuwaingiza walimu wa vyuo binafsi vya uuguzi na ukunga kwenye mpango wa mkataba na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
 
 “Na hili linawezekana tukiwa kama wadau wa serikali, kwa sababu wahitimu wetu huajiriwa na wizara na kupangiwa kufanya kazi katika maeneo karibu yote nchini,” alisema.
 
Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo, Profesa Paulina Meela, aliwataka wahitimu hao wakafanye kazi kwa kuzingatia miiko na maadili kama walivyofundishwa.
 
Jumla ya wanafunzi 23 wa Stashahada ya uuguzi na ukunga inayochukua miaka mitatu na wanafunzi 17 wa cheti cha miaka miwili, walihitimu mafunzo hayo.
 
CHANZO: NIPASHE

Kwa wanavyuo wote watanzania popote Duniani Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. Tumieni mtandao huu ni wenu nyote.

No comments: